Waziri Kindiki Alalamikia Malipo duni kwa Wanahabari, huku akitaka  wapewe Mishahara Bora

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki Jumatano, alitoa wito wa kukaguliwa upya kwa masharti ya malipo ya wanahabari nchini.

Akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani, Prof Kindiki alisema maelfu ya waandishi wa habari wanaendelea kuangazia masuala yanayoathiri jamii kila siku “lakini wanakosa hata huduma za kimsingi za kibinadamu kwa sababu ya malipo duni kutoka kwa watendaji na wamiliki wa vyombo vya habari wasiojali hali na kuiona kuwa kawaida.”

Kindiki alitoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawapa waandishi wa habari malipo yanaolingana na kazi zao za siku na gharama ya maisha ya leo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo huo alibainisha tishio kwa usalama wa kibinafsi wa wanahabari wa Kenya na kuahidi kwamba wizara yake haitasita kuwaadhibu wale wanaotishia wanahabari katika safu yao ya kazi.

Maadhimisho ya Mei 3 kila mwaka, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ilitangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuhamasisha umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari na kuzikumbusha serikali wajibu wao wa kuheshimu na kudumisha haki ya uhuru wa kujieleza.

Haki ya uhuru wa kujieleza imewekwa chini ya Kifungu cha 19 cha Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu la 1948.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kuunda Mustakabali wa Haki: Uhuru wa Kujieleza kama kichocheo cha haki zingine zote za binadamu”.

.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *