• Mbunge huyo hakufurahishwa na mapendekezo ya hivi majuzi katika mswada wa fedha unliowasilishwa bungeni.
• “Mimi mshahara wangu wote nimechukua mikopo utakata nini napata sifuri tu au unataka kuchukua mali yangu?” alilalamika.
Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amemkosoa Rais Ruto kuhusiana na pendekezo la kuongeza ushuru katika mswada wa fedha wa 2023.
Kama ilivyo na Wakenya wengine wengi, mbunge huyo anayepokea mshahara mnono kwa mwezi hakufurahishwa na mapendekezo ya hivi majuzi katika mswada wa fedha unliowasilishwa bungeni.
“Bw. Rais Ruto, wewe ndiye baba wa taifa. Lakini unapoleta 35% ya ushuru iliyopendekezwa kwa watu wenye mshahara wa zaidi ya laki 500, ushuru wa hazina ya nyumba katika Mswada wa Fedha unawaumiza Wakenya ambao tayari wanapokea mishahara midogo,” mbunge huyo wa muhula wa kwanza alisema.
Pia alilalamikia jinsi mabadiliko yanayopendekezwa yanavyoweza kumuathiri akidai kwamba mshahara anaorejea nao nyumbani baada ya kulipa mikopo yake ni mdogo.
“Mimi mshahara wangu wote nimechukua mikopo utakata nini napata sifuri tu au unataka kuchukua mali yangu?”
“Nilikuwa nikipata Sh34k na hata hizo zimeisha, nimeziweka kwenye miradi. Payslip yangu sio kitu. Ninaishi tu kwa posho ndogo ninazopata ninapoenda kwenye mikutano na pesa ya ‘Milleage’ ninapoenda kuangalia wananchi”
Kiongozi huyo wa zamani wa chuo cha Egerton aliendelea kumsihi rais afikirie upya kuhusu hazina ya ujenzi wa nyumba ambayo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa Wakenya na akamtaka azingatie ushuru wa faida ya mtaji badala yake.
“Bw. Ruto tafadhali uwahurumie Wakenya hawa. Watoze watu wanaonunua mali na nyumba.Toza pesa kwa watu wanaonunua nyumba kwa pesa taslimu, achana na watu wanaonunua kwa mkopo…hao watumishi wa serikali hawana lolote!“
Wahurumie! Hata hiyo 3%…Hao ni hustlers. Toza ushuru kwa faida ya mtaji. Nitaenda kwa Hazina kuzungumza na CS Njuguna ili kumfundisha baadhi ya mambo ya uchumi ambayo nilijifunza huko Egerton kitambo,” alilalamika.