Idadi ya waliofariki Shakahola yapanda hadi 242 huku msako na uokoaji ukiendelea

•Maafisa wa polisi wangali wanapata maiti zilizotapakaa msituni baada ya zoezi la uchimbaji kusimamishwa ili kupisha uchunguzi wa maiti.

•”Hatukuweza kubaini sababu za vifo vya miili 20 lakini miili kumi na miwili ilikuwa na dalili za njaa,” Oduor alisema.

Mwili wa mwanamke ulipatikana Jumatatu kwenye kichaka cha msitu mkubwa wa Shakahola wakati wa operesheni ya utafutaji na uokoaji ya polisi.

Maafisa wa polisi wangali wanapata maiti zilizotapakaa msituni baada ya zoezi la uchimbaji kusimamishwa ili kupisha uchunguzi wa maiti.

Idadi ya waliofariki sasa imefikia 242. Mwathiriwa mwingine pia aliokolewa Jumatatu, na kufanya idadi hiyo kufikia 93.

Wapelelezi pia wamefanya uchunguzi wa maiti 79 ndani ya siku tatu kati ya 129 zilizokuwa zimeratibiwa kufanyika.

Wiki iliyopita pekee mifupa mitano ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi waliokufa na mili kuharibika ilipatikana msituni.

Hadi sasa uchunguzi wa maiti bado unaendelea na unatarajiwa kukamilika Jumatano wiki hii ili timu hiyo ianze awamu ya tatu ya ufukuaji.

Siku ya Jumatatu wapelelezi na wanapatholojia wanaofanya uchunguzi wa maiti walifanikiwa kufanya uchunguzi 34 wa miili iliyotolewa kutoka Shakahola.

Akizungumza wakati wa kikao cha kila siku katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, daktari mkuu wa magonjwa ya serikali Johansen Oduor alisema miili hiyo ilijumuisha wanawake 21 na wanaume 10, huku miili mitatu,  jinsia haikuweza kujulikana kwa sababu ilikuwa imeharibika vibaya.

“Hatukuweza kubaini sababu za vifo vya miili 20 lakini miili kumi na miwili ilikuwa na dalili za njaa,” alisema.

Oduor alisema timu hiyo iligundua kuwa miili 32 kati ya hiyo ilikuwa imeharibika vibaya, huku miwili kati yao ikiwa imeharibika kiasi.

Mwanapatholojia huyo alisema waligundua kuwa wengi walikuwa wameoza vibaya sana, hawakuweza kupata chanzo cha kifo kati yao 22 huku kati yao 12 walipata sifa zinazofanana na njaa.

“Kwa kuwa miili mingi ilikuwa haijatambulika, tulichukua sampuli kwa ajili ya vipimo zaidi ambavyo Mkemia wa Serikali angetumia kwa minasaba ya DNA ili waweze kutambuliwa,” alisema.

Zoezi hilo huenda likamalizika wiki hii ili awamu ya tatu ya uchimbaji wa kaburi ianze.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *